Usuluhishi wa Migogoro (Dispute Resolution)
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limekuwa likiratibu utatuzi wa migogoro katika sekta ya ujenzi tangu mwaka 1982 kupitia mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro (Alternative Dispute Resolution – ADR).
Katika kutekeleza jukumu hili, Baraza husajili na kuandaa orodha ya wataalamu wa usuluhishi wa migogoro katika sekta ya ujenzi ambao hutumiwa na wadau katika kutatua migogoro inayotokana na mikataba ya ujenzi. Aidha, utatuzi wa migogoro hufanyika kwa kuzingatia miongozo na kanuni zilizowekwa na Baraza.
Majukumu ya NCC yameainishwa katika Kifungu cha 4 cha Sheria ya National Construction Council Act, Cap. 162 (R.E. 2023). Mojawapo ya majukumu hayo ni kuwezesha utatuzi wa migogoro inayotokana na shughuli za sekta ya ujenzi.
Huduma za Utatuzi wa Migogoro Zinazoratibiwa na NCC
NCC huratibu mbinu mbili za utatuzi wa migogoro ambazo hutegemea makubaliano yaliyowekwa katika mkataba wa wahusika.
UAMUZI (Adjudication)
Ni njia ya haraka ya kutatua migogoro ambapo Adjudicator hutoa uamuzi wa kitaalamu unaotekelezwa mara moja na wahusika. Uamuzi huo hubaki kuwa na nguvu hadi utakapobadilishwa au kufutwa kupitia Arbitration Award.
USULUHISHI (Arbitration)
Ni utatuzi wa mgogoro unaofanywa na Arbitrator, ambaye ni mtu wa tatu huru anayetoa uamuzi wa mwisho unaowafunga wahusika wote.
Sheria na Kanuni Zinazotumika
Utatuzi wa migogoro kupitia NCC unaongozwa na sheria na kanuni zifuatazo:
- Arbitration Act, Cap. 15, R.E. 2023
- Arbitration (Rules of Procedure) Regulations, GN No.146 of 2021
- NCC Arbitration Rules, 2001
- NCC Adjudication Rules, 2017
Masharti ya Kufungua Shauri
Ili kufungua shauri kupitia NCC, mhusika anatakiwa kuhakikisha kuwa:
- Ana mkataba halali wa ujenzi dhidi ya upande mwingine.
- Mkataba una kifungu cha Adjudication au Arbitration.
- Mkataba umeitaja NCC kama Appointing Authority.
- Muda wa kisheria wa kufungua shauri haujaisha.
- Hatua zote za usuluhishi zilizowekwa kwenye mkataba (ikiwa zipo) zimetekelezwa.
Taratibu za Kuanzisha Shauri
Mchakato wa kuanzisha shauri unahusisha hatua zifuatazo:
Hatua ya 1
Wasilisha taarifa kwa maandishi kwa NCC kuhusu nia ya kufungua shauri.
Hatua ya 2
Lipa ada ya kufungua shauri ya TZS 300,000.
Hatua ya 3
Taarifa huwasilishwa kwa upande wa pili.
Hatua ya 4
Upande wa pili hupewa nafasi ya kuwasilisha majibu yake.
Hatua ya 5
NCC hutoa orodha ya wasuluhishi waliosajiliwa.
Hatua ya 6
Wahusika humchagua msuluhishi kutoka kwenye orodha hiyo.
Hatua ya 7
Msuluhishi hupokea taarifa rasmi ya uteuzi wake.
Hatua ya 8
Usikilizwaji wa shauri huanza hadi kutolewa kwa uamuzi.
Namna ya Kuwa Msuluhishi wa NCC
A. MUAMUZI (Adjudicator)
Mwombaji anatakiwa:
- Kuwasilisha maombi ya usajili NCC.
- Awe na taaluma ya Uhandisi, Usanifu Majengo au Ukadiriaji Majenzi.
- Awe amesajiliwa katika bodi husika.
- Awe na uzoefu usiopungua miaka 5.
- Awe na maarifa ya kutosha katika sekta ya ujenzi.
- Awe amehudhuria na kufaulu mafunzo ya Adjudication yanayotolewa na NCC.
B. MSULUHISHI (Arbitrator)
Mwombaji anatakiwa:
- Awe amepata Accreditation kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.
- Kuwasilisha maombi ya usajili NCC.
- Awe na taaluma ya Uhandisi, Sheria, Usanifu au Quantity Surveying.
- Awe amesajiliwa katika chombo husika.
- Awe na uzoefu usiopungua miaka 5.
- Awe na uzoefu katika Arbitration, Adjudication, Mediation au ADR.
- Awe amehudhuria mafunzo ya Arbitration yanayotolewa na NCC.
Gharama za Shauri
Gharama za uendeshaji wa shauri hugharamiwa na pande zote mbili kwa uwiano sawa isipokuwa pale ambapo msuluhishi au mkataba utaelekeza vinginevyo.